11 September, 2012

Upendo Kilahiro: Nilikataa uraia wa Canada, Afrika Kusini

Leo hii baadhi ya watu wanamawazo ya kuondoka nchini na kwenda nchi za ughaibuni kutokana na kile wanachodai kuwa Tanzania ni nchi masikini hivyo maisha ya hapa ni ya shida na wala hayana starehe zozote hata kama unapesa. Hilo halipo kwa watu hohe hahe ambao baadhi yao wamekuwa wakizamia meli kwenda nchi za ng’ambo, la hasha hata watu wenye pesa baadhi yao wamebadili uraia ama kuishi nje ya Tanzania kutokana na kunogewa na raha za maeneo wanayoona kwao yanafaa kuishi. Baadhi yao wamekuwa wakitumia gharama kubwa ili kuhakikisha wanaihama Tanzania. Kuna mifano mingi tu ambayo baadhi ya wanamuziki hasa wa muziki wa kidunia, wanaishi nje ya nchi baada ya kunogewa na maisha ya maeneo husika na kuona kwao si kitu. Lakini kuna wengine licha ya nchi yetu kuonekana si kitu katika ukuaji wa uchumi na mambo mengine, bado wainaithamini hata kama watapewa uraia wa bure na nchi ambayo walienda kufanya kazi na wakaonekana wanafaa. Miongoni mwa watu hao wenye mapenzi mema na nchi yao ni muimbaji wa kimataifa wa  muziki wa Injili nchini, Upendo Kilahiro ambaye kwa sasa masikani yake yapo jijini Dar es Salaam. Mtumishi huyo wa Mungu,  huduma yake ya uimbaji imefanyika baraka kubwa katika nchi mbalimbali za dunia, jambo lililomfanya kupata fursa ya kukabidhiwa uraia wa bure katika baadhi ya nchi hizo ambazo ameweza kufanya huduma. Hata hivyo, kutokana na mapenzi mema na nchi yake, Upendo alikataa kuisaliti nchi yake (Tanzania)  kwa sababu ya mapenzi mema aliyokuwa nayo katika taifa lake. Kuna kipindi Upendo aliishi muda mrefu Afrika Kusini akitoa huduma ya uimbaji na alifanikiwa kuiteka nchi hiyo hali iliyosababisha mkali wa muziki wa Injili nchini humo, Rebeka Malope kumuomba abadili uraia ili wafanye kazi pamoja. Hata hivyo, alikataa ofa hiyo na kuamua kurudi nyumbani kabla ya  Canada nao kumuomba afanye hivyo wakati alipokuwa akifanya huduma nchini humo.   Kutokana na hali hiyo Malope alimuomba kuwa msemaji wake katika ukanda wa Afrika Mashariki kazi anayoifanya mpaka sasa. Huduma ya Upendo naweza kusema ipo tofauti na waimbaji wengine wa muziki wa Injili kwa maana pamoja na mambo mengine lakini amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa jamii yake anaisaidia kwa kiwango anachokiona kinastahili. “Ni kweli kutokana na kuishi muda mrefu nchini Afrika Kusini baadhi ya raia wan chi hiyo walikuwa wakinisihi niombe uraia wa nchi hiyo lakini mimi niliwaambia kuwa ni Mtanzania na sitoweza kuisaliti nchi yangu hata kama ipo vipi.” Sababu hiyo ndiyo ilimfanya kujitoa kwa ajili ya watu wenye matatizo hasa wagonjwa na watoto yatima ambao wengi wao hawana uwezo wa kumudu kupata mahitaji muhimu katika maisha ikiwemo matibabu. Kutokana na mzigo huo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilimuona kuwa anaweza kuwafaa katika kazi ya kuhamasisha upatikanaji  wa afya bora hasa kwa wanawake na watoto wa Kitanzania na kutokana  na hilo lilimchagua kuwa balozi wa Afrika na Desemba mwaka huu atakutana na mabalozi wenzake kutoka kila pembe ya dunia. Ili kuthibitisha hilo, Upendo kwa kushirikiana na Taasisi ya Christian Directory & Consultancy, hivi karibuni alifanya tamasha kubwa la muziki wa Injili lililofanyika mkoani Arusha, lililokuwa na lengo la kuchangisha fedha za kuwasaidia wagonjwa wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, ambalo lilikwenda sanjari  na utambulisho wa Albamu yake iitwayo ‘Asante Yesu’. Akizungumzia kiini cha kufanyika kwa tamasha hilo, msemaji wa  Christian Directory & Consultancy,  Noel Tenga alisema kuwa waliamua kufanya  tamasha hilo ili kutoa nguvu yao katika kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum. Tuliamua kufanya jambo tofauti katika tasnia hii ya muziki wa Injili hapa Tanzania,  lakini kubwa kuliko yote ni kuhakikisha kuwa tunatoa kile tulichokuwa nacho kwa ajili ya watu wenye matatizo mbalimbali ikiwemo saratani.

No comments:

Post a Comment